12
Hotuba Ya Nne Ya Ayubu
Ayubu Anajibu: Mimi Ni Mtu Wa Kuchekwa
1 Ndipo Ayubu akajibu:
2 “Bila shaka ninyi ndio watu,
nayo hekima itakoma mtakapokufa!
3 Lakini mimi ninao ufahamu kama ninyi;
mimi si duni kwenu.
Ni nani asiyejua mambo haya yote?
4 “Nimekuwa mtu wa kuchekwa na rafiki zangu,
ingawa nilimwita Mungu naye akanijibu:
mimi ni mtu wa kuchekwa tu,
ingawa ni mwadilifu na nisiye na hatia!
5 Wanadamu wakiwa katika utulivu huwa na dharau kwa wale wenye msiba
kana kwamba ndiyo haki ya wale ambao miguu yao inateleza.
6 Hema za wanyangʼanyi hazisumbuliwi,
wale wanaomghadhibisha Mungu wako salama:
wale wamchukuao mungu wao mikononi mwao.
7 “Lakini ulizeni wanyama, nao watawafundisha,
au ndege wa angani, nao watawaambia;
8 au zungumzeni na dunia, nayo itawafundisha,
au acheni samaki wa baharini wawape taarifa.
9 Ni nani miongoni mwa hawa wote asiyejua
kwamba mkono wa Bwana ndio uliofanya hili?
10 Mkononi mwake kuna uhai wa kila kiumbe,
na pumzi ya wanadamu wote.
11 Je, sikio haliyajaribu maneno
kama vile ulimi uonjavyo chakula?
12 Je, hekima haipatikani katikati ya wazee?
Je, maisha marefu hayaleti ufahamu?
13 “Hekima na nguvu ni vya Mungu;
shauri na ufahamu ni vyake yeye.
14 Kile anachokibomoa hakiwezi kujengeka tena;
mtu aliyefungiwa naye hawezi kufunguliwa.
15 Akizuia maji, huwa pana ukame;
akiyaachia maji, huharibu nchi.
16 Kwake kuna nguvu na ushindi;
adanganywaye na adanganyaye, wote wawili ni wake.
17 Yeye huwaondoa washauri wakiwa wametekwa nyara,
naye huwapumbaza wanaotoa maamuzi.
18 Huondoa pingu zilizofungwa na wafalme,
na kuwafunga mishipi ya kiunoni.
19 Huwaondoa makuhani wakiwa wametekwa nyara,
na kuwaangusha waliojiimarisha muda mrefu.
20 Hunyamazisha midomo ya washauri wanaoaminika,
na kuondoa busara ya wazee.
21 Huwamwagia dharau wanaoheshimika,
na kuwavua silaha wenye nguvu.
22 Hufunua mambo ya ndani ya gizani,
na kuyaleta nuruni yale yaliyositirika sana.
23 Huyafanya mataifa yatukuke na kuyaangamiza;
hufanya mataifa kuwa makubwa, naye huyatawanya.
24 Huwaondolea viongozi wa nchi akili zao;
huwapeleka watangetange nyikani pasipo na njia.
25 Hupapasa gizani pasipokuwa na mwanga;
huwafanya wapepesuke kama walevi.