11
Sofari Anasema: Hatia Ya Ayubu Inastahili Adhabu
1 Ndipo Sofari Mnaamathi akajibu:
2 “Je, maneno haya yote yapite bila kujibiwa?
Je, huyu mnenaji athibitishwe kuwa na haki?
3 Je, maneno yako ya upuzi yawafanye watu wanyamaze kimya?
Je, mtu asikukemee unapofanya dhihaka?
4 Unamwambia Mungu, ‘Imani yangu ni kamili
nami ni safi mbele zako.’
5 Aha! Laiti kwamba Mungu angesema,
kwamba angefungua midomo yake dhidi yako,
6 naye akufunulie siri za hekima,
kwa kuwa hekima ya kweli ina pande mbili.
Ujue hili: Mungu amesahau hata baadhi ya dhambi zako.
7 “Je, waweza kujua siri za Mungu?
Je, waweza kuyachunguza mambo yote kumhusu Mwenyezi?
8 Ni juu mno kuliko mbingu: waweza kufanya nini?
Kina chake ni kirefu kuliko kuzimu:
wewe waweza kujua nini?
9 Kipimo chake ni kirefu kuliko dunia,
nacho ni kipana kuliko bahari.
10 “Kama akija na kukufunga gerezani,
na kuitisha mahakama, ni nani awezaye kumpinga?
11 Hakika anawatambua watu wadanganyifu;
naye aonapo uovu, je, haangalii?
12 Mpumbavu aweza kuwa mwenye hekima,
endapo mtoto wa punda-mwitu atazaliwa mwanadamu.
13 “Hata sasa ukiutoa moyo wako kwake
na kumwinulia mikono yako,
14 ukiiondolea mbali ile dhambi iliyo mkononi mwako
wala usiuruhusu uovu ukae hemani mwako,
15 ndipo utainua uso wako bila aibu;
utasimama imara bila hofu.
16 Hakika utaisahau taabu yako,
utaikumbuka tu kama maji yaliyokwisha kupita.
17 Maisha yako yatangʼaa kuliko adhuhuri,
nalo giza litakuwa kama alfajiri.
18 Utakuwa salama, kwa kuwa lipo tumaini;
utatazama pande zote na kupumzika kwa salama.
19 Utalala, wala hakuna atakayekuogofya,
naam, wengi watajipendekeza kwako.
20 Bali macho ya waovu hayataona,
wokovu utawaepuka;
tarajio lao litakuwa ni hangaiko
la mtu anayekata roho.”