8
1 watu wote wakakusanyika kama mtu mmoja kwenye uwanja mbele ya Lango la Maji. Wakamwambia Ezra mwandishi alete Kitabu cha Sheria ya Mose, ambacho Bwana aliamuru kwa ajili ya Israeli.
2 Basi katika siku ya kwanza ya mwezi wa saba, kuhani Ezra akaleta Sheria mbele ya kusanyiko, ambamo walikuwamo wanaume, wanawake na watu wote walioweza kufahamu. 3 Akaisoma kwa sauti kubwa tangu mapambazuko mpaka adhuhuri, akiwa ameuelekea uwanja uliokuwa mbele ya Lango la Maji mbele ya wanaume, wanawake na wengine ambao waliweza kufahamu. Watu wote wakasikiliza kwa makini kile Kitabu cha Sheria.
4 Mwandishi Ezra alikuwa amesimama juu ya jukwaa la miti lililojengwa kwa kusudi hilo. Karibu naye upande wa kuume alisimama Matithia, Shema, Anaya, Uria, Hilkia na Maaseya. Upande wake wa kushoto walikuwepo Pedaya, Mishaeli, Malkiya, Hashumu, Hashbadani, Zekaria na Meshulamu.
5 Ezra akakifungua kile kitabu. Watu wote waliweza kumwona kwa sababu alikuwa amesimama juu zaidi, naye alipokifungua watu wote wakasimama. 6 Ezra akamsifu Bwana, Mungu mkuu, nao watu wote wakainua mikono yao na kuitikia, “Amen! Amen!” Kisha wakasujudu na kumwabudu Bwana hali nyuso zao zikigusa ardhi.
7 Watu wakiwa wamesimama pale, Walawi wafuatao waliwafunza ile Sheria: Yeshua, Bani, Sherebia, Yamini, Akubu, Shabethai, Hodia, Maaseya, Kelita, Azaria, Yozabadi, Hanani na Pelaya. 8 Walisoma kutoka kile Kitabu cha Sheria ya Mungu, wakiifafanua na kuwapa maelezo ili watu waweze kufahamu kile kilichokuwa kikisomwa.
9 Ndipo Nehemia aliyekuwa mtawala,* Au Tirshatha: jina la heshima aliloitwa mtawala wa Yuda chini ya Ufalme wa Uajemi. Ezra kuhani na mwandishi, pamoja na Walawi waliokuwa wakiwafundisha watu wakawaambia wote, “Siku hii ni takatifu kwa Bwana Mungu wenu. Msiomboleze wala msilie.” Kwa kuwa watu wote walikuwa wakilia walipokuwa wakisikiliza maneno ya ile Sheria.
10 Nehemia akasema, “Nendeni mkafurahie chakula kizuri na vinywaji vitamu, na mpeleke sehemu kwa wale ambao hawana chochote cha kula. Siku hii ni takatifu kwa Bwana. Msihuzunike, kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu.”
11 Walawi wakawatuliza watu wote wakisema, “Kuweni watulivu, kwa kuwa hii ni siku takatifu. Msihuzunike.”
12 Kisha watu wote wakaondoka kwenda kula na kunywa, na kupeana sehemu ya chakula, na wakaadhimisha kwa furaha kubwa, kwa sababu sasa walifahamu maneno yale waliyokuwa wameelezwa.
13 Katika siku ya pili ya mwezi, wakuu wa mbari zote, pamoja na makuhani na Walawi, walikusanyika wakimzunguka Ezra mwandishi ili wapate kusikiliza kwa makini maneno ya Sheria. 14 Wakakuta imeandikwa katika ile Sheria, ambayo Bwana aliiamuru kupitia kwa Mose, kwamba Waisraeli walipaswa kukaa katika vibanda wakati wa sikukuu ya mwezi wa saba, 15 na kwamba walipaswa kutangaza neno hili na kulieneza katika miji yao na katika Yerusalemu wakisema: “Enendeni katika nchi ya mlima na kuleta matawi kutoka miti ya mizeituni, mizeituni mwitu, mihadasi, mitende na miti ya kivuli, ili kutengeneza vibanda,” kama ilivyoandikwa.
16 Basi watu wakaenda na kuleta matawi, nao wakajijengea vibanda juu ya paa za nyumba zao, katika nyua zao, katika nyua za nyumba ya Mungu, na katika uwanja karibu na Lango la Maji na uwanja wa Lango la Efraimu. 17 Jamii yote ya watu waliorudi kutoka utumwani wakajenga vibanda na kuishi ndani yake. Tangu wakati wa Yoshua mwana wa Nuni mpaka siku ile, Waisraeli hawakuwahi kuiadhimisha namna hii. Furaha yao ilikuwa kubwa sana.
18 Siku baada ya siku, kuanzia siku ya kwanza hadi ya mwisho, Ezra alisoma kutoka kwenye kile Kitabu cha Sheria ya Mungu. Wakaiadhimisha sikukuu ile kwa siku saba, nayo siku ya nane, kufuatana na maagizo, kulikuwa na kusanyiko maalum.