9
Ibada Katika Hema La Kidunia
Basi agano lile la kwanza lilikuwa na kanuni zake za kuabudu na pia patakatifu pake pa kidunia. Hema ilitengenezwa. Katika sehemu yake ya kwanza kulikuwa na kinara cha taa, meza na mikate iliyowekwa wakfu; hii sehemu iliitwa Mahali Patakatifu. Nyuma ya pazia la pili, palikuwa na sehemu iliyoitwa Patakatifu pa Patakatifu, ambapo palikuwa na yale madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba, na lile Sanduku la Agano lililofunikwa kwa dhahabu. Sanduku hili lilikuwa na gudulia la dhahabu lenye mana, ile fimbo ya Aroni iliyochipuka, na vile vibao vya mawe vya Agano. Juu ya lile Sanduku kulikuwa na makerubi ya Utukufu yakitilia kivuli kile kifuniko ambacho ndicho kiti cha rehema. Lakini hatuwezi kueleza vitu hivi kwa undani sasa.
Basi vitu hivi vilipokuwa vimepangwa, makuhani waliingia daima katika sehemu ya kwanza ya hema ili kufanya taratibu zao za ibada. Lakini ni kuhani mkuu peke yake aliyeingia ndani ya sehemu ya pili ya hema. Tena hii ilikuwa mara moja tu kwa mwaka, na hakuingia kamwe bila damu, ambayo alitoa kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya dhambi za watu walizotenda bila kukusudia. Kwa njia hii, Roho Mtakatifu alikuwa anaonyesha kwamba, maadamu ile hema ya kwanza ilikuwa bado imesimama, njia ya kuingia Patakatifu pa Patakafifu ilikuwa bado haijafunguliwa. Huu ulikuwa mfano kwa ajili ya wakati wa sasa, kuonyesha kwamba sadaka na dhabihu zilizokuwa zikitolewa hazikuweza kusafisha dhamiri ya mtu anayeabudu. 10 Lakini hizi zilishughulika tu na vyakula na vinywaji, pamoja na taratibu mbalimbali za kunawa kwa nje, kanuni kwa ajili ya mwili zilizowekwa hadi wakati utimie wa matengenezo mapya.
Damu Ya Kristo
11 Kristo alipokuja akiwa Kuhani Mkuu wa mambo mema ambayo tayari yameshawasili, alipitia kwenye hema iliyo kuu zaidi na bora zaidi, ambayo haikutengenezwa kwa mikono ya binadamu, hii ni kusema, ambayo si sehemu ya uumbaji huu. 12 Hakuingia kwa njia ya damu ya mbuzi na ya ndama; lakini aliingia Patakatifu pa Patakatifu mara moja tu kwa damu yake mwenyewe, akiisha kupata ukombozi wa milele. 13 Damu ya mbuzi na ya mafahali, na majivu ya mitamba walivyonyunyiziwa wale waliokuwa najisi kwa taratibu za kiibada viliwatakasa, hata kuwaondolea uchafu wa nje. 14 Basi ni zaidi aje damu ya Kristo, ambaye kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na waa, itatusafisha dhamiri zetu kutokana na matendo yaletayo mauti, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai!
15 Kwa sababu hii Kristo ni mpatanishi wa agano jipya, ili kwamba wale walioitwa waweze kupokea ile ahadi ya urithi wa milele: kwa vile yeye alikufa awe ukombozi wao kutoka kwa dhambi walizozitenda chini ya agano la kwanza.
16 Kwa habari ya wosia,* Wosia hapa kwa neno la Kiyunani ni agano. ni muhimu kuthibitisha kifo cha yule aliyeutoa, 17 kwa sababu wosia huwa na nguvu tu wakati mtu ameshakufa; kamwe hauwezi kutumika wakati yule aliyeuandika bado yuko hai. 18 Hii ndiyo sababu hata lile agano la kwanza halikuweza kutekelezwa pasipo damu. 19 Mose alipotangaza kila amri kwa watu wote, alichukua damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji, sufu nyekundu na matawi ya mti wa hisopo, akanyunyizia kile kitabu na watu wote. 20 Alisema, “Hii ndiyo damu ya agano, ambalo Mungu amewaamuru kulitii.” 21 Vivyo hivyo alinyunyizia damu hiyo kwenye ile hema pamoja na kila kifaa kilichotumika ndani yake kwa taratibu za ibada. 22 Kwa kweli sheria hudai kwamba, karibu kila kitu kitakaswe kwa damu, wala pasipo kumwaga damu, hakuna msamaha wa dhambi.
23 Kwa hiyo, ilikuwa muhimu kwa nakala za vitu vile vya mbinguni vitakaswe kwa dhabihu hizi, lakini vitu halisi vya mbinguni vilihitaji dhabihu bora kuliko hizi. 24 Kwa maana Kristo hakuingia kwenye patakatifu palipofanywa kwa mikono ya mwanadamu, ambao ni mfano wa kile kilicho halisi. Yeye aliingia mbinguni penyewe, ili sasa aonekane mbele za Mungu kwa ajili yetu. 25 Wala hakuingia mbinguni ili apate kujitoa mwenyewe mara kwa mara, kama vile kuhani mkuu aingiavyo Patakatifu pa Patakatifu kila mwaka kwa damu ambayo si yake mwenyewe. 26 Ingekuwa hivyo, ingempasa Kristo kuteswa mara nyingi tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Lakini sasa ametokea mara moja tu katika mwisho wa nyakati aiondoe dhambi kwa kujitoa mwenyewe kuwa dhabihu. 27 Kama vile mwanadamu alivyowekewa kufa mara moja tu na baada ya kufa akabili hukumu, 28 vivyo hivyo Kristo alitolewa mara moja tu kuwa dhabihu ili azichukue dhambi za watu wengi. Naye atakuja mara ya pili, sio kuchukua dhambi, bali kuwaletea wokovu wale wanaomngoja kwa shauku.

*9:16 Wosia hapa kwa neno la Kiyunani ni agano.