Yohana
1
1 Mwanzoni kulikuwako Neno, na Neno alikuwa pamoja na Mungu, na Neno alikuwa Mungu. 2 Huyu, Neno, Mwanzoni alikuwa pamoja na Mungu. 3 Vitu vyote vilifanyika kupitia yeye, na pasipo yeye hakuna hata kitu kimoja kilichokuwa kimefanyika. 4 Ndani yake kulikuwa uzima, na huo uzima ulikuwa nuru ya wanadamu wote. 5 Nuru yang'aa gizani, wala giza halikuizimisha. 6 Palikuwa na mtu aliyetumwa kutoka kwa Mungu, ambaye jina lake alikuwa Yohana. 7 Alikuja kama shahidi kushuhudia kuhusu ile nuru, ili kwamba wote waweze kuamini kupitia yeye. 8 Yohana hakuwa ile nuru, bali alikuja ili ashuhudie kuhusu ile nuru 9 Hiyo ilikuwa nuru ya kweli ambayo ilikuwa inakuja katika dunia nayo humtia nuru kila mmoja 10 Alikuwa katika dunia, na dunia iliumbwa kupitia yeye, na dunia haikumjua. 11 Alikuja kwa vitu vyake, na watu wake hawakumpokea. 12 Bali kwa wale wengi waliompokea, ambao waliamini jina lake, kwa hao aliwapa haki ya kuwa wana wa Mungu, 13 Ambao walizaliwa, sio kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili, wala kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu mwenyewe. 14 Naye Neno alifanyika mwili na akaishi miongoni mwetu, tumeuona utukufu wake, utukufu kama wa mtu pekee wa kipekee aliyekuja kutoka kwa Baba, amejaa neema na kweli. 15 Yohana alishuhudia kuhusu yeye, na alipaza sauti akisema, “Huyu ndiye ambaye nilisema habari zake nikisema, “Yule ajaye baada yangu ni mkuu kuliko mimi, kwa sababu amekuwako kabla yangu.” 16 Kwa kuwa kutoka katika utimilifu wake, sisi sote tumepokea bure kipawa baada ya kipawa. 17 Kwa kuwa sheria ililetwa kupitia Musa. Neema na kweli vilikuja kupitia Yesu Kristo. 18 Hakuna mwanadamu aliyemwona Mungu wakati wowote. Mtu pekee ambaye ni Mungu, aliye katika kifua cha Baba, amemfanya yeye ajulikane. 19 Na huu ndio ushuhuda wa Yohana wakati makuhani na walawi waliotumwa kwake na Wayahudi kumwuliza, “Wewe ni nani?” 20 Bila kusitasita na hakukana, bali alijibu, “Mimi sio Kristo.” 21 Hivyo wakamuuliza, “kwa hiyo wewe ni nani sasa?” Wewe ni Eliya? Akasema, “Mimi siye.” Wakasema, Wewe ni nabii? Akajibu,” Hapana.” 22 Kisha wakamwambia, “Wewe ni nani, ili kwamba tuwape jibu waliotutuma”? Wajishuhudiaje wewe mwenyewe?” 23 Akasema, “Mimi ni sauti yake aliaye nyikani: 'Inyosheni njia ya Bwana,' kama nabii Isaya alivyosema.” 24 Basi kulikuwa na watu wametumwa pale kutoka kwa Mafarisayo. Wakamuuliza na kusema, 25 “Kwa nini unabatiza basi kama wewe sio Kristo wala Eliya wala nabii?” 26 Yohana aliwajibu akisema, “Ninabatiza kwa maji. Hata hivyo, miongoni mwenu anasimama mtu msiyemtambua. 27 Huyu ndiye ajaye baada yangu. Mimi sisitahili kulegeza kamba za viatu vyake.” 28 Mambo haya yalitendeka huko Bethania, ng'ambo ya Yordani, mahali ambapo Yohana alikuwa akibatiza. 29 Siku iliyofuata Yohana alimwona Yesu akija kwake akasema, “ Tazama mwanakondoo wa Mungu aichukuae dhambi ya ulimwengu! 30 huyu ndiye niliyesema habari zake nikisema, “Yeye ajaye nyuma yangu ni mkuu kuliko mimi, kwa kuwa alikuwa kabla yangu.' 31 Sikumtambua yeye, lakini ilifanyika hivyo ili kwamba afunuliwe katika Israeli, kwamba nilikuja nikibatiza kwa maji.” 32 Yohana alishuhudia, “Niliona Roho akishuka kutoka mbinguni mfano wa hua, na ilibaki juu yake. 33 Mimi sikumtambua lakini yeye aliyenituma ili nibatize kwa maji aliniambia, 'yule ambaye utaona Roho akishuka na kukaa juu yake, Huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu.' 34 Nimeona na nimeshuhudia kwamba huyu ni Mwana wa Mungu.” 35 Tena siku iliyofuata Yohana alikuwa amesimama pamoja na wanafunzi wake wawili, 36 walimwona Yesu akitembea na Yohana akasema, “Tazama, Mwana kondoo wa Mungu!” 37 Wanafunzi wawili walimsikia Yohana akisema haya wakamfuata Yesu. 38 Tena Yesu aligeuka na kuwaona wanafunzi wale wakimfuata, na akawambia, “Mnataka nini?” Wakajibu, “Rabbi, (maana yake 'mwalimu,' unaishi wapi?” 39 Akawambia, “Njooni na mwone.”Kisha walikwenda na kuona mahali alipokuwa akiishi; walikaa pamoja naye siku hiyo, kwa kuwa ilikuwa yapata kama saa kumi hivi. 40 Mmoja wa wale wawili waliomsikia Yohana akiongea na kisha kumfuata Yesu alikuwa ni Andrea, ndugu yake Simoni Petro. 41 Akamwona ndugu yake Simoni na akamwambia, “Tumempata Masihi” (ambayo inatafsiriwa Kristo). 42 Akamleta kwa Yesu. Yesu akamtazama na akasema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohana” utaitwa Kefa,” (maana yake 'Petro'). 43 Siku iliyofuata wakati Yesu alipotaka kuondoka kwenda Galilaya, alimpata Filipo na akamwambia, “Nifuate mimi.” 44 Filipo alikuwa ni mwenyeji wa Bethsaida, mji wa Andrea na Petro. 45 Filipo alimpata Nathanaeli na kumwambia, Tumempata yule ambaye Musa aliandika habari zake katika sheria na Manabii. Yesu mwana wa Yusufu, kutoka Nazareti. 46 Nathanaeli akamwambia, “Je kitu chema chaweza kutokea Nazareti?” Filipo akamwambia, Njoo na uone.” 47 Yesu akamwona Nathanaeli akija kwake na akasema, “Tazama, Mwisraeli kweli kweli asiye na udanganyifu ndani yake!” 48 Nathanaeli akamwambia, “Umenifahamuje mimi?” Yesu akajibu na akamwambia, “Kabla Filipo hajakuita ulipokuwa chini ya mtini, nalikuona.” 49 Nathanaeli akajibu, “Rabi wewe u Mwana wa Mungu! Wewe ni Mfalme wa Israeli”! 50 Yesu akajibu akamwambia, Kwa sababu nilikuambia 'nilikuona chini ya mtini' je waamini? utaona matendo makubwa kuliko haya.” 51 Yesu akasema, “Amini amini nawambieni mtaziona mbingu zikifunguka, na kuwaona malaika wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.”