Waraka wa Yakobo
1
Yakobo, mtumwa wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo, kwa makabila kumi na mbili yaliyotawanyika, salaam. Hesabuni kuwa ni furaha zaidi, ndugu zangu, mnapopita katika matatizo mbali mbali, mkijua kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huwapa uvumilivu. Acheni uvumilivu uikamilishe kazi yake, kwamba muweze kukomaa kikamilifu, bila kupungukiwa katika lolote. Lakini kama mtu kati yenu anahitaji hekima, aiombe kutoka kwa Mungu, ambaye hutoa kwa ukarimu na pasipo kukemea kwa wote wamwombao, na atawapa hekima. Lakini omba kwa imani, bila shaka, kwa kuwa mwenye kutia shaka ni kama mawimbi katika bahari, huchukuliwa na upepo na kutupwa huku na huko. Kwa hakika mtu huyu asifikirie kwamba atapokelewa ombi lake kutoka kwa Bwana; mtu huyu ana nia mbili, si imara katika njia zake zote. Ndugu maskini anapaswa kujivuna katika kusimama kwake juu, 10 wakati huo huo ndugu tajiri katika unyenyekevu wake, kwa sababu atatoweka kama ua la kondeni katika shamba analopita. 11 Jua huchomoza na joto la kuunguza kukausha mimea, na maua huanguka na uzuri wake hufa. Vivyo hivyo watu matajiri watachakaa katikati ya kazi zao. 12 Amebarikiwa mtu yule anayevumilia majaribu, kwa kuwa baada ya kushinda jaribu hilo, atapokea taji ya uzima, ambayo imeahidiwa kwa wale wampendao Mungu. 13 Mtu yeyote hapaswi kusema anapojaribiwa, “Jaribu hili linatoka kwa Mungu,” kwa sababu Mungu hajaribiwi na uovu, na Mungu mwenyewe hamjaribu yeyote. 14 Kila mtu hujaribiwa na tamaa zake mbaya zinazomshawishi na kumvuta mbali. 15 Ndipo baada ya tamaa ya dhambi kubeba mimba, dhambi huzaliwa, na baada ya dhambi kukomaa sawasawa, huishia katika mauti. 16 Ndugu zangu wapendwa, msidanganyike. 17 Kila zawadi iliyo nzuri na kila zawadi iliyokamilika hutoka juu, hushuka chini kutoka kwa Baba wa nuru. Kamwe habadiliki kama kivuli kibadilikavyo. 18 Mungu alichagua kutupa sisi uzima kwa Neno la kweli, ili kwamba tuweze kuwa kama uzao wa kwanza miongoni mwa viumbe vyake. 19 Mnajua hili, ndugu zangu wapendwa. Kila mmoja anapaswa kuwa mwepesi wa kusikia, siyo mwepesi wa kuongea wala kukasirika, 20 kwa kuwa hasira ya mwanadamu haiwezi kutenda haki ya Mungu. 21 Kwa hiyo wekeni mbali uchafu wa dhambi na ubaya wote ulio mahali popote, na kwa unyenyekevu lipokeeni neno lililopandwa ndani yenu, ambalo lina uwezo wa kuokoa roho zenu. 22 Litiini neno, msilisikie tu, mkijidanganya nafsi zenu wenyewe. 23 Kwa kuwa kama yeyote alisikiaye neno bila kulitendea kazi ni sawa na mtu ajiangaliaye uso wake halisi katika kioo. 24 Hujitathimini uso wake, na huenda zake na baada ya muda mfupi husahau anavyofanana. 25 Bali mtu yule anayeiangalia kwa uangalifu sheria kamili, sheria ya uhuru, na kuendelea kuitii, si kwa sababu yeye ni msikilizaji anayesahau, huyu mtu atabarikiwa anapoitenda. 26 Ikiwa mtu yeyote atafikiri mwenyewe kuwa ni mtu wa dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, huudanganya moyo wake na dini yake ni bure. 27 Dini iliyo safi na isiyoharibiwa mbele za Mungu wetu na Baba ni hii: kuwasaidia yatima na wajane katika mateso yao, na kujilinda wenyewe na ufisadi wa dunia.