11
Agano Limevunjwa
Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Bwana: “Sikia maneno ya agano hili, nawe uwaambie watu wa Yuda na wale waishio Yerusalemu. Waambie kwamba hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Amelaaniwa mtu ambaye hatayatii maneno ya agano hili, maneno niliyowaamuru baba zenu nilipowatoa katika nchi ya Misri, kutoka tanuru la kuyeyushia vyuma.’ Nilisema, ‘Nitiini mimi na mfanye kila kitu ninachowaamuru, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu. Kisha nitatimiza kiapo nilichowaapia baba zenu, kuwapa nchi itiririkayo maziwa na asali,’ nchi ambayo mnaimiliki leo.”
Nikajibu, “Amen, Bwana.”
Bwana akaniambia, “Tangaza maneno haya yote katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu: ‘Sikilizeni maneno ya agano hili na kuyafuata. Tangu wakati ule niliwapandisha baba zenu kutoka Misri mpaka leo, niliwaonya tena na tena, nikisema “Nitiini mimi.” Lakini hawakusikiliza wala kujali. Badala yake, walifuata ukaidi wa mioyo yao miovu. Hivyo nikaleta juu yao laana zote za agano nililokuwa nimewaamuru wao kulifuata, lakini wao hawakulishika.’ ”
Kisha Bwana akaniambia, “Kuna shauri baya linaloendelea miongoni mwa watu wa Yuda na wale wanaoishi Yerusalemu. 10 Wamerudia dhambi za baba zao, waliokataa kusikiliza maneno yangu. Wameifuata miungu mingine kuitumikia. Nyumba zote mbili za Israeli na Yuda zimelivunja agano nililofanya na baba zao. 11 Kwa hivyo, hili ndilo asemalo Bwana: ‘Nitaleta juu yao maafa ambayo hawawezi kuyakimbia. Hata kama wakinililia, sitawasikiliza. 12 Miji ya Yuda na watu wa Yerusalemu watakwenda kuililia miungu ambayo wameifukizia uvumba, lakini haitawasaidia kamwe wakati maafa yatakapowapiga. 13 Mnayo miungu mingi kama miji mliyo nayo, ee Yuda, nazo madhabahu mlizozijenga za kufukizia uvumba huyo mungu wa aibu Baali ni nyingi kama barabara za Yerusalemu.’
14 “Wewe usiwaombee watu hawa wala kufanya maombezi yoyote au kunisihi kwa ajili yao, kwa sababu sitawasikiliza watakaponiita wakati wa taabu yao.
15 “Mpenzi wangu anafanya nini hekaluni mwangu,
anapofanya mashauri yake maovu na wengi?
Je, nyama iliyowekwa wakfu yaweza
kuondolea mbali adhabu yako?
Unapojiingiza katika ubaya wako,
ndipo unashangilia.”
 
16  Bwana alikuita mti wa mzeituni uliostawi
ulio na matunda mazuri kwa sura.
Lakini kwa ngurumo ya mawimbi makuu
atautia moto,
nayo matawi yake yatavunjika.
17  Bwana Mwenye Nguvu Zote, aliyekupanda, ametamka maafa kwa ajili yako, kwa sababu nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda mmefanya maovu na kunikasirisha kwa kumfukizia Baali uvumba.
Shauri Baya Dhidi Ya Yeremia
18 Kwa sababu Bwana alinifunulia hila zao mbaya, nilizifahamu, kwa kuwa wakati ule alinionyesha yale waliyokuwa wanayafanya. 19 Nilikuwa kama mwana-kondoo mpole aliyeongozwa machinjoni; mimi sikutambua kwamba walikuwa wamefanya shauri baya dhidi yangu, wakisema,
“Sisi na tuuangamize mti na matunda yake;
nasi tumkatilie mbali kutoka nchi ya walio hai,
ili jina lake lisikumbukwe tena.”
20 Lakini, Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, wewe uhukumuye kwa haki,
nawe uchunguzaye moyo na akili,
wacha nione ukiwalipiza wao kisasi,
kwa maana kwako nimeweka shauri langu.
21 “Kwa hiyo hili ndilo Bwana asemalo kuhusu watu wa Anathothi wale wanaotafuta uhai wako wakisema, ‘Usitoe unabii kwa jina la Bwana, la sivyo utakufa kwa mikono yetu’: 22 kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo: ‘Nitawaadhibu. Vijana wao waume watakufa kwa upanga, wana wao na binti zao kwa njaa. 23 Hawatasaziwa hata mabaki kwao, kwa sababu nitaleta maafa kwa watu wa Anathothi katika mwaka wa adhabu yao.’ ”