Ayubu
Sehemu Ya Kwanza: Habari Za Awali
1
(Ayubu 1–2)
Ayubu Na Jamaa Yake
Katika nchi ya Usi paliishi mtu ambaye aliitwa Ayubu. Mtu huyu alikuwa hana hatia, naye alikuwa mkamilifu; alimcha Mungu na kuepukana na uovu. Alikuwa na wana saba na binti watatu, naye alikuwa na kondoo elfu saba, ngamia elfu tatu, jozi mia tano za maksai, na punda mia tano, tena alikuwa na idadi kubwa ya watumishi. Alikuwa mtu mkuu sana miongoni mwa watu wa Mashariki.
Wanawe walikuwa na desturi ya kufanya karamu katika nyumba zao kwa zamu, nao wangewaalika umbu zao watatu ili kula na kunywa pamoja nao. Wakati kipindi cha karamu kilimalizika, Ayubu angetuma waitwe na kuwafanyia utakaso. Angetoa dhabihu ya sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya kila mmoja wao asubuhi na mapema, akifikiri, “Pengine wanangu wametenda dhambi na kumlaani Mungu mioyoni mwao.” Hii ilikuwa ndiyo desturi ya kawaida ya Ayubu.
Jaribu La Kwanza La Ayubu
Siku moja wana wa Mungu* Wana wa Mungu hapa ina maana malaika au viumbe vya mbinguni. walikwenda kujionyesha mbele za Bwana. Shetani Shetani hapa ina maana ya mshtaki wa watakatifu. naye akaja pamoja nao. Bwana akamwambia Shetani, “Umetoka wapi?”
Shetani akamjibu Bwana, “Natoka kuzunguka pote duniani, nikitembea huku na huko humo.”
Ndipo Bwana akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Hakuna mtu mwingine duniani aliye kama yeye, asiye na hatia, ni mnyofu, mwenye kumcha Mungu, na kuepukana na uovu.”
Shetani akamjibu Bwana, “Je, Ayubu anamcha Mungu bure? 10 Je, wewe hukumjengea boma pande zote yeye na wa nyumbani mwake pamoja na kila kitu alicho nacho? Kazi za mikono yake umezibariki na hivyo makundi yake ya kondoo na mbuzi pamoja na ya wanyama yameenea katika nchi nzima. 11 Lakini nyoosha mkono wako na kupiga kila kitu alicho nacho, naye kwa hakika atakulaani mbele za uso wako.”
12  Bwana akamwambia Shetani, “Vema sana, kwa hiyo, kila kitu alicho nacho kiko mikononi mwako, lakini juu ya huyo mtu mwenyewe usimguse hata kwa kidole.”
Ndipo Shetani akatoka mbele za Bwana.
13 Siku moja watoto wa Ayubu walipokuwa wakifanya karamu wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, 14 akaja mjumbe kwa Ayubu na kusema, “Maksai walikuwa wakilima na punda walikuwa wakilisha karibu nao, 15 Waseba wakawashambulia na kuchukua mifugo. Kisha wakawaua watumishi kwa upanga, nami ndimi peke yangu niliyenusurika kukuletea habari!”
16 Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Moto wa Mungu ulishuka kutoka mbinguni na kuteketeza kondoo na watumishi, nami ndimi peke yangu niliyenusurika kukuletea habari!”
17 Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Wakaldayo waliunda vikosi vitatu vya uvamizi na kuwaangukia ngamia wako na kuwachukua wakaondoka nao. Wakawaua watumishi kwa upanga, nami ndimi peke yangu niliyenusurika kukuletea habari.”
18 Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Wana wako na binti zako walipokuwa wakifanya karamu, wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, 19 ghafula upepo wenye nguvu ukavuma kutoka jangwani, nao ukaipiga nyumba hiyo pembe zake nne. Ikawaangukia hao watoto nao wamekufa, nami ndimi peke yangu niliyenusurika kukuletea habari!”
20 Ndipo Ayubu akasimama, akararua joho lake na kunyoa nywele zake. Kisha akaanguka chini katika kuabudu 21 na kusema:
“Nilitoka tumboni mwa mama yangu uchi,
nami nitaondoka uchi, Au: nitarudi huko uchi.
Bwana alinipa, naye Bwana ameviondoa,
jina la Bwana litukuzwe.”
22 Katika mambo haya yote, Ayubu hakutenda dhambi kwa kumlaumu Mungu kwa kufanya ubaya.

*1:6 Wana wa Mungu hapa ina maana malaika au viumbe vya mbinguni.

1:6 Shetani hapa ina maana ya mshtaki wa watakatifu.

1:21 Au: nitarudi huko uchi.