Wahebrania
1
1 Nyakati zilizopita Mungu alizungumza na mababu zetu kupitia manabii mara nyingi na kwa njia nyingi. 2 Lakini katika siku hizi tulizonazo, Mungu ameongea nasi kupitia Mwana, ambaye alimweka kuwa mrithi wa vitu vyote, na ambaye kupitia yeye pia aliumba ulimwengu. 3 Mwanawe ni nuru ya utukufu wake, tabia pekee ya asili yake, na anayeendeleza vitu vyote kwa neno la nguvu zake. Baada ya kukamilisha utakaso wa dhambi, aliketi chini mkono wa kulia wa enzi huko juu. 4 Amekuwa bora kuliko malaika, kama vile jina alilolirithi lilivyo bora zaidi kuliko jina lao. 5 Kwa maana ni kwa malaika gani aliwahi kusema, “Wewe ni mwanangu, leo nimekuwa baba yako?” Na tena, “Nitakuwa baba kwake, naye atakuwa mwana kwangu?” 6 Tena, wakati Mungu alipomleta mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, husema, “Malaika wote wa Mungu lazima wamwabudu.” 7 Kuhusu malaika asema, “Yeye ambaye hufanya malaika zake kuwa roho, na watumishi wake kuwa ndimi za moto.” 8 Lakini kuhusu Mwana husema, “Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele. Fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya haki. 9 Umependa haki na kuchukia uvunjaji wa sheria, kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekupaka mafuta ya furaha kuliko wenzako.” 10 Hapo mwanzo, Bwana, uliweka msingi wa dunia. Mbingu ni kazi za mikono yako. 11 Zitatoweka, lakini wewe utaendelea. Zote zitachakaa kama vazi. 12 Utazikunjakunja kama koti, nazo zitabadilika kama vazi. Lakini wewe ni yuleyule, na miaka yako haitakoma.” 13 Lakini ni kwa malaika yupi Mungu alisema wakati wowote, “Keti mkono wangu wa kulia mpaka nitakapowafanya adui zako kuwa kiti cha miguu yako”? 14 Je, malaika wote siyo roho zilizotumwa kuwahudumia na kuwatunza wale watakaourithi wokovu?