3
1 Wapenzi wangu, hii ni barua ya pili ninayowaandikia. Katika barua hizo mbili nimejaribu kufufua fikira safi akilini mwenu kwa kuwakumbusheni mambo haya. 2 Napenda mkumbuke maneno yaliyosemwa na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na Mwokozi mliyopewa na mitume wenu. 3 Awali ya yote jueni kwamba siku za mwisho watakuja watu ambao mienendo yao inatawaliwa na tamaa zao mbaya. Watawadhihaki ninyi 4 na kusema: “Aliahidi kwamba atakuja! Je, sasa yuko wapi? Mambo ni yaleyale tangu babu zetu walipokufa; hali ya vitu ni ileile kama ilivyokuwa mwanzo wa ulimwengu!” 5 Watu hao, kwa makusudi, husahau kwamba zamani Mungu alinena, nazo mbingu na nchi zikaumbwa. Dunia iliumbwa kutoka katika maji na kwa maji; 6 na kwa maji hayo, yaani yale maji ya gharika kuu, dunia ya wakati ule iliangamizwa. 7 Lakini mbingu na nchi za sasa zahifadhiwa kwa neno la Mungu kwa ajili ya kuharibiwa kwa moto. Zimewekwa kwa ajili ya Siku ile ambapo watu wasiomcha Mungu watahukumiwa na kuangamizwa. 8 Lakini, wapenzi wangu, msisahau kitu kimoja! Mbele ya Bwana, hakuna tofauti kati ya siku moja na miaka elfu; kwake yote ni mamoja. 9 Bwana hakawii kutimiza yale aliyoahidi kama watu wengine wanavyofikiri kuwa atakawia. Yeye ana saburi kwa ajili yenu, maana hapendi hata mmoja wenu apotee, bali huwavuta wote wapate kutubu. 10 Siku ya Bwana itakuja kama mwizi. Siku hiyo, mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; vitu vyake vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia itatoweka pamoja na kila kitu kilichomo ndani yake. 11 Maadamu kila kitu kitaharibiwa namna hiyo, je, ninyi mnapaswa kuwa watu wa namna gani? Mnapaswa kuishi kitakatifu na kumcha Mungu, 12 mkiingojea Siku ile ya Mungu na kuifanya ije upesi—Siku ambayo mbingu zitateketezwa kwa moto na kuharibiwa, na vitu vyake vya asili vitayeyushwa kwa joto. 13 Lakini sisi, kufuatana na ahadi yake, twangojea mbingu mpya na dunia mpya ambayo imejaa uadilifu. 14 Kwa hiyo wapenzi wangu, mkiwa mnangojea Siku ile, fanyeni bidii kuwa safi kabisa bila hatia mbele ya Mungu, na kuwa na amani naye. 15 Mnapaswa kuuona uvumilivu wa Bwana kuwa ni nafasi anayowapeni mpate kuokolewa, kama Paulo ndugu yetu mpenzi alivyowaandikia akitumia hekima aliyopewa na Mungu. 16 Hayo ndiyo asemayo katika barua zake zote anapozungumzia suala hilo. Yapo mambo kadhaa katika barua zake yaliyo magumu kuyaelewa, mambo ambayo watu wajinga, wasio na msimamo, huyapotosha kama wanavyopotosha sehemu nyingine za Maandiko Matakatifu. Hivyo wanasababisha maangamizi yao wenyewe. 17 Lakini ninyi, wapenzi wangu, mmekwisha jua jambo hili. Basi, muwe na tahadhari msije mkapotoshwa na makosa ya waasi, mkaanguka kutoka katika msimamo wenu imara. 18 Lakini endeleeni kukua katika neema na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu uwe kwake, sasa na hata milele! Amina.