19
Afadhali mtu maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama,
kuliko mpumbavu ambaye midomo yake imepotoka.
 
Sio vizuri kuwa na juhudi bila maarifa,
wala kufanya haraka na kuikosa njia.
 
Upumbavu wa mtu mwenyewe huharibu maisha yake
hata hivyo moyo wake humkasirikia Bwana.
 
Mali huleta marafiki wengi,
bali rafiki wa mtu maskini humwacha.
 
Shahidi wa uongo hataacha kuadhibiwa,
naye amwagaye uongo hataachwa huru.
 
Wengi hujipendekeza kwa mtawala
na kila mmoja ni rafiki wa mtu atoaye zawadi.
 
Mtu maskini huepukwa na ndugu zake wote:
Je, marafiki zake watamkwepa kiasi gani!
Ingawa huwafuata kwa kuwasihi,
hawapatikani popote.
 
Yeye apataye hekima huipenda nafsi yake mwenyewe,
yeye ahifadhiye ufahamu hustawi.
 
Shahidi wa uongo hataacha kuadhibiwa,
naye amwagaye uongo ataangamia.
 
10 Haistahili mpumbavu kuishi katika anasa,
itakuwa vibaya kiasi gani
kwa mtumwa kuwatawala wakuu.
 
11 Hekima ya mtu humpa uvumilivu,
ni kwa utukufu wake kusamehe makosa.
 
12 Ghadhabu ya mfalme ni kama mngurumo wa simba,
bali wema wake ni kama umande juu ya nyasi.
 
13 Mwana mpumbavu ni maangamizi ya babaye,
naye mke mgomvi ni kama kutonatona kusikoisha.
 
14 Nyumba na mali hurithiwa kutoka kwa wazazi,
bali mke mwenye busara hutoka kwa Bwana.
 
15 Uvivu huleta usingizi mzito,
naye mtu mzembe huona njaa.
 
16 Yeye ambaye hutii mafundisho huulinda uhai wake,
bali yeye anayezidharau njia zake atakufa.
 
17 Yeye amhurumiaye maskini humkopesha Bwana,
naye atamtuza kwa aliyotenda.
 
18 Mrudi mwanao, kwa maana katika hiyo kuna tumaini,
usiwe mshirika katika mauti yake.
 
19 Mtu mwenye kukasirika haraka ni lazima atapata adhabu yake,
kama utamwokoa, itakubidi kufanya hivyo tena.
 
20 Sikiliza mashauri na ukubali mafundisho,
nawe mwishoni utakuwa na hekima.
 
21 Kuna mipango mingi ndani ya moyo wa mtu,
lakini kusudi la Bwana ndilo litakalosimama.
 
22 Lile mtu alionealo shauku ni upendo usio na mwisho,
afadhali kuwa maskini kuliko kuwa mwongo.
 
23 Kumcha Bwana huongoza kwenye uzima,
kisha mtu hupumzika akiwa ameridhika,
bila kuguswa na shida.
 
24 Mtu mvivu hutumbukiza mkono wake kwenye sahani,
lakini hawezi hata kuupeleka kwenye kinywa chake!
 
25 Mpige mwenye mzaha, naye mjinga atajifunza busara,
mkemee mwenye ufahamu naye atapata maarifa.
 
26 Yeye amwibiaye baba yake na kumfukuza mama yake
ni mwana aletaye aibu na fedheha.
 
27 Mwanangu, ukiacha kusikiliza mafundisho,
utatangatanga mbali na maneno ya maarifa.
 
28 Shahidi mla rushwa hudhihaki hukumu
na kinywa cha mtu mwovu humeza ubaya kwa upesi.
 
29 Adhabu zimeandaliwa kwa ajili ya wenye dhihaka
na mapigo kwa ajili ya migongo ya wapumbavu.