15
Mgawo Kwa Yuda
1 Mgawo kwa kabila la Yuda, ulienea ukoo kwa ukoo, ukishuka kufikia eneo la Edomu, hadi Jangwa la Sini mwisho kabisa upande wa kusini.
2 Mpaka wao wa kusini ulianzia kwenye ghuba iliyoko kwenye ncha ya kusini mwa Bahari ya Chumvi, 3 ukakatiza kusini mwa Akrabimu, ukaendelea hadi Sini ukaenda hadi kusini mwa Kadesh-Barnea. Tena ukapitia Hesroni ukapanda hadi Adari na ukapinda hadi Karka. 4 Kisha ukaendelea mpaka Azmoni na kuunganika na Kijito cha Misri, na kuishia baharini. Huu ndio mpaka wao wa upande wa kusini.
5 Mpaka wa upande wa mashariki ni Bahari ya Chumvi ukienea mahali Mto Yordani unapoingilia.
Mpaka wa upande wa kaskazini ulianzia penye ghuba ya bahari mahali Mto Yordani unapoingilia, 6 ukapanda hadi Beth-Hogla, na kuendelea kaskazini mwa Beth-Araba hadi kwenye Jiwe la Bohani mwana wa Reubeni. 7 Kisha mpaka ulipanda hadi Debiri kutoka Bonde la Akori na kugeuka kaskazini hadi Gilgali inayotazamana na materemko ya Adumimu, kusini mwa bonde. Ukaendelea sambamba hadi maji ya En-Shemeshi na kutokeza huko En-Rogeli. 8 Kisha ukapanda kwa kufuata Bonde la Ben-Hinomu sambamba na mteremko wa kusini wa mji mkubwa wa Wayebusi (yaani Yerusalemu). Kutoka hapo ukapanda juu ya kilima magharibi ya Bonde la Hinomu mwisho wa ncha ya kaskazini mwa Bonde la Warefai. 9 Kutoka juu ya kilima mpaka ule ukaendelea hadi kwenye chemchemi ya maji ya Neftoa, ukatokea kwenye miji ya Mlima Efroni na kuteremka kuelekea Baala (yaani Kiriath-Yearimu). 10 Kisha ukapinda upande wa magharibi kutoka Baala hadi Mlima Seiri, ukafuatia sambamba mteremko wa kaskazini mwa Mlima Yearimu (yaani Kesaloni), ukaendelea chini hadi Beth-Shemeshi na kukatiza hadi Timna. 11 Ukaelekea hadi kwenye mteremko wa kaskazini mwa Ekroni, ukageuka kuelekea Shikeroni, ukapita hadi Mlima Baala na kufika Yabineeli. Mpaka ule ukaishia baharini.
12 Mpaka wa magharibi ni pwani ya Bahari Kuu.
Hii ndiyo mipaka ya watu wa Yuda kwa koo zao.
Nchi Aliyopewa Kalebu
(Waamuzi 1:11-15)
13 Kwa kufuata maagizo ya Bwana kwake, Yoshua alimpa Kalebu mwana wa Yefune sehemu katika Yuda: Kiriath-Arba, yaani Hebroni (Arba alikuwa baba wa zamani wa Anaki). 14 Kutoka Hebroni Kalebu alifukuza hao wana watatu wa Anaki, nao ni Sheshai, Ahimani na Talmai, wazao wa Anaki. 15 Kutoka hapo akaondoka kupigana dhidi ya watu walioishi Debiri (jina la Debiri hapo kwanza uliitwa Kiriath-Seferi). 16 Kalebu akasema, “Nitamwoza binti yangu Aksa kwa mtu atakayeweza kupigana na kuteka Kiriath-Seferi.” 17 Basi Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu yake Kalebu, akauteka; hivyo Kalebu akamtoa Aksa binti yake aolewe naye.
18 Siku moja Aksa alipokuja kwa Othnieli, alimsihi Othnieli amwombe baba yake, Kalebu, shamba. Aksa aliposhuka kutoka juu ya punda wake, Kalebu akamuuliza, “Je, wataka nikufanyie nini?”
19 Akamjibu, “Naomba unifanyie jambo moja la hisani. Kwa kuwa umenipa ardhi huko Negebu, nipe pia chemchemi za maji.” Basi Kalebu akampa chemchemi za juu na za chini.
Miji Ya Yuda
20 Huu ndio urithi wa kabila la Yuda, ukoo kwa ukoo:
21 Miji ya kusini kabisa ya kabila la Yuda katika Negebu kuelekea mpaka wa Edomu ilikuwa:
Kabseeli, Ederi, Yaguri, 22 Kina, Dimona, Adada, 23 Kedeshi, Hazori, Ithnani, 24 Zifu, Telemu, Bealothi, 25 Hazor-Hadata, Kerioth-Hezroni (yaani Hazori), 26 Amamu, Shema, Molada, 27 Hasar-Gada, Heshmoni, Beth-Peleti, 28 Hasar-Shuali, Beer-Sheba, Biziothia, 29 Baala, Iyimu, Esemu, 30 Eltoladi, Kesili, Horma, 31 Siklagi, Madmana, Sansana, 32 Lebaothi, Shilhimu, Aini na Rimoni; hiyo yote ni miji ishirini na tisa, pamoja na vijiji vyake.
33 Kwenye shefela ya magharibi:
Eshtaoli, Sora, Ashna, 34 Zanoa, En-Ganimu, Tapua, Enamu, 35 Yarmuthi, Adulamu, Soko, Azeka, 36 Shaaraimu, Adithaimu na Gedera (au Gederothaimu); yote ni miji kumi na minne, pamoja na vijiji vyake.
37 Senani, Hadasha, Migdal-Gadi, 38 Dileani, Mispa, Yoktheeli, 39 Lakishi, Boskathi, Egloni, 40 Kaboni, Lamasi, Kitlishi, 41 Gederothi, Beth-Dagoni, Naama na Makeda; yote ni miji kumi na sita pamoja na vijiji vyake.
42 Libna, Etheri, Ashani, 43 Yifta, Ashna, Nesibu, 44 Keila, Akzibu na Maresha; yote ni miji tisa pamoja na vijiji vyake.
45 Ekroni, pamoja na viunga vyake na vijiji vyake; 46 magharibi ya Ekroni, maeneo yote yaliyokuwa karibu na Ashdodi, pamoja na vijiji vyake; 47 Ashdodi, miji yake na vijiji vyake na Gaza viunga vyake na vijiji vyake, hadi kufikia Kijito cha Misri na Pwani ya Bahari Kuu.
48 Katika nchi ya vilima:
Shamiri, Yatiri, Soko, 49 Dana, Kiriath-Sana (yaani Debiri), 50 Anabu, Eshtemoa, Animu, 51 Gosheni, Holoni na Gilo; miji kumi na mmoja pamoja na vijiji vyake.
52 Arabu, Duma, Ashani, 53 Yanimu, Beth-Tapua, Afeka, 54 Humta, Kiriath-Arba (yaani Hebroni), na Siori; miji tisa pamoja na vijiji vyake.
55 Maoni, Karmeli, Zifu, Yuta, 56 Yezreeli, Yokdeamu, Zanoa, 57 Kaini, Gibea na Timna; miji kumi pamoja na vijiji vyake.
58 Halhuli, Beth-Suri, Gedori, 59 Maarathi, Beth-Anothi na Eltekoni; miji sita pamoja na vijiji vyake.
60 Kiriath-Baali (yaani Kiriath-Yearimu) na Raba; miji miwili pamoja na vijiji vyake.
61 Huko jangwani:
Beth-Araba, Midini, Sekaka, 62 Nibshani, Mji wa Chumvi, na En-Gedi; miji sita pamoja na vijiji vyake.
63 Yuda hakuweza kuwafukuza Wayebusi, waliokuwa wakiishi Yerusalemu; hadi leo Wayebusi huishi huko pamoja na watu wa Yuda.