9
Laiti kichwa changu kingekuwa chemchemi ya maji
na macho yangu yangekuwa kisima cha machozi!
Ningelia usiku na mchana
kwa kuuawa kwa watu wangu.
Laiti ningekuwa na nyumba
ya kukaa wasafiri jangwani,
ningewaacha watu wangu
na kwenda mbali nao,
kwa kuwa wote ni wazinzi,
kundi la watu wadanganyifu.
 
“Huweka tayari ndimi zao kama upinde,
ili kurusha uongo;
wamekuwa na nguvu katika nchi
lakini si katika ukweli.
Wanatoka dhambi moja hadi nyingine,
hawanitambui mimi,”
asema Bwana.
“Jihadhari na rafiki zako;
usiwaamini ndugu zako.
Kwa kuwa kila ndugu ni mdanganyifu,
na kila rafiki ni msingiziaji.
Rafiki humdanganya rafiki,
hakuna yeyote asemaye kweli.
Wamefundisha ndimi zao kudanganya,
wanajichosha wenyewe katika kutenda dhambi.
Unakaa katikati ya udanganyifu;
katika udanganyifu wao wanakataa kunitambua mimi,”
asema Bwana.
Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote:
“Tazama, nitawasafisha na kuwajaribu,
kwani ni nini kingine niwezacho kufanya
kwa sababu ya dhambi ya watu wangu?
Ndimi zao ni mshale wenye sumu,
hunena kwa udanganyifu.
Kwa kinywa chake kila mmoja huzungumza maneno mazuri na jirani yake,
lakini moyoni mwake humtegea mtego.
Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya jambo hili?”
asema Bwana.
“Je, nisijilipizie kisasi
kwa taifa kama hili?”
 
10 Nitalia na kuomboleza kwa ajili ya milima
na kuomboleza kuhusu malisho ya jangwani.
Yamekuwa ukiwa, wala hakuna apitaye humo,
milio ya ngʼombe haisikiki.
Ndege wa angani wametoroka
na wanyama wamekimbia.
 
11 “Nitaifanya Yerusalemu lundo la magofu,
makao ya mbweha;
nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa
ili asiwepo atakayeishi humo.”
12 Ni mtu yupi aliye na hekima ya kutosha ayaelewe haya? Ni nani aliyefundishwa na Bwana awezaye kuyaeleza haya? Kwa nini nchi imeharibiwa na kufanywa ukiwa kama jangwa ambapo hakuna awezaye kupita?
13  Bwana akasema, “Ni kwa sababu wameiacha sheria yangu, niliyoiweka mbele yao: hawajaniheshimu mimi wala kufuata sheria yangu. 14 Badala yake wamefuata ukaidi wa mioyo yao, wamefuata Mabaali, kama vile baba zao walivyowafundisha.” 15 Kwa hiyo, hivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: “Tazama, nitawafanya watu hawa wale chakula kichungu na kunywa maji yenye sumu. 16 Nitawatawanya katika mataifa ambayo wao wala baba zao hawakuwajua, nikiwafuata kwa upanga mpaka niwe nimewaangamiza kabisa.”
 
17 Hivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote:
“Fikiri sasa! Waite wanawake waombolezao waje,
waite wale walio na ustadi kuliko wote.
18 Nao waje upesi
na kutuombolezea,
mpaka macho yetu yafurike machozi
na vijito vya maji vitoke kwenye kope zetu.
19 Sauti ya kuomboleza imesikika kutoka Sayuni:
‘Tazama jinsi tulivyoangamizwa!
Tazama jinsi aibu yetu ilivyo kubwa!
Ni lazima tuihame nchi yetu
kwa sababu nyumba zetu zimekuwa magofu.’ ”
 
20 Basi, enyi wanawake, sikieni neno la Bwana;
fungueni masikio yenu msikie maneno ya kinywa chake.
Wafundisheni binti zenu kuomboleza;
fundishaneni kila mmoja na mwenzake maombolezo.
21 Mauti imeingia ndani kupitia madirishani,
imeingia kwenye majumba yetu ya fahari;
imewakatilia mbali watoto katika barabara
na vijana waume kutoka viwanja vya miji.
22 Sema, “Hili ndilo asemalo Bwana:
“ ‘Maiti za wanaume zitalala
kama mavi katika mashamba,
kama malundo ya nafaka nyuma ya mvunaji,
wala hakuna anayekusanya.’ ”
23 Hili ndilo asemalo Bwana:
“Mwenye hekima asijisifu katika hekima yake,
au mwenye nguvu ajisifu katika nguvu zake,
wala tajiri ajisifu katika utajiri wake,
24 lakini yeye ajisifuye, na ajisifu kwa sababu hili:
kwamba ananifahamu na kunijua mimi,
kwamba mimi ndimi Bwana, nitendaye wema,
hukumu na haki duniani,
kwa kuwa napendezwa na haya,”
asema Bwana.
25 “Siku zinakuja, nitakapowaadhibu wale wote ambao wametahiriwa kimwili tu, asema Bwana, 26 yaani Misri, Yuda, Edomu, Amoni, Moabu na wote wanaoishi jangwani sehemu za mbali. Kwa maana mataifa haya yote hayakutahiriwa mioyo yao, nayo nyumba yote ya Israeli haikutahiriwa.”