5
Wimbo Wa Debora
1 Ndipo Debora na Baraka mwana wa Abinoamu wakaimba wimbo huu:
2 “Wakuu katika Israeli wanapoongoza,
wakati watu wanapojitoa
kwa hiari yao wenyewe:
mhimidini Bwana!
3 “Sikieni hili, enyi wafalme!
Sikilizeni, enyi watawala!
Nitamwimbia Bwana, nitaimba;
kwa wimbo nitamhimidi Bwana,
Mungu wa Israeli.
4 “Ee Bwana, ulipotoka katika Seiri,
ulipopita katika mashamba ya Edomu,
nchi ilitetemeka, mbingu nazo zikamwaga,
naam, mawingu yakamwaga maji.
5 Milima ilitetemeka mbele za Bwana,
hata ule wa Sinai,
mbele za Bwana,
Mungu wa Israeli.
6 “Katika siku za Shamgari mwana wa Anathi,
katika siku za Yaeli,
barabara kuu hazikuwa na watu;
wasafiri walipita njia za kando.
7 Mashujaa walikoma katika Israeli,
walikoma mpaka mimi, Debora, nilipoinuka,
nilipoinuka kama mama katika Israeli.
8 Walipochagua miungu migeni,
vita vilikuja katika malango ya mji,
hapakuonekana ngao wala mkuki
miongoni mwa mashujaa 40,000 katika Israeli.
9 Moyo wangu u pamoja na wakuu wa Israeli,
pamoja na wale wanaojitoa wenyewe
kwa hiari yao miongoni mwa watu.
Mhimidini Bwana!
10 “Nanyi mpandao punda weupe,
mkiketi juu ya matandiko ya thamani,
nanyi mtembeao barabarani,
fikirini 11 juu ya sauti za waimbaji
mahali pa kunyweshea maji.
Wanasimulia matendo ya haki ya Bwana,
matendo ya haki ya mashujaa wake
katika Israeli.
“Ndipo watu wa Bwana
walipoteremka malangoni pa mji.
12 ‘Amka, amka! Debora!
Amka, amka, uimbe!
Ee Baraka! Inuka,
chukua mateka wako uliowateka,
ee mwana wa Abinoamu.’
13 “Ndipo mabaki ya watu
wakashuka dhidi ya wenye nguvu,
watu wa Bwana,
wakashuka dhidi ya mashujaa wenye nguvu.
14 Kutoka Efraimu wakaja watu, ambao chimbuko lao ni Amaleki;
Benyamini akiwa miongoni
mwa watu waliokufuata.
Kutoka Makiri wakashuka viongozi,
na kutoka Zabuloni wale washikao
fimbo ya jemadari.
15 Wakuu wa Isakari walikuwa pamoja na Debora;
naam, Isakari alikuwa pamoja na Baraka,
wakija nyuma yake kwa mbio
wakielekea bondeni.
Katika jamaa za Reubeni,
palikuwa na kujihoji kukubwa moyoni.
16 Kwa nini ulikaa katikati ya mazizi ya kondoo
kusikiliza sauti ya filimbi zinazoita makundi?
Kwa jamaa za Reubeni,
palikuwa na kujihoji kukubwa moyoni.
17 Gileadi alikaa ngʼambo ya Yordani.
Naye Dani, kwa nini alikaa
kwenye merikebu siku nyingi?
Asheri alikaa kwa utulivu ufuoni mwa bahari,
akikaa kwenye ghuba zake ndogo.
18 Watu wa Zabuloni walihatarisha maisha yao,
vilevile nao watu wa Naftali.
19 “Wafalme walikuja na kufanya vita;
wafalme wa Kanaani walipigana
huko Taanaki karibu na maji ya Megido,
lakini hawakuchukua fedha wala nyara.
20 Kutoka mbinguni nyota zilipigana,
nyota kutoka njia zake
zilipigana na Sisera.
21 Mto wa Kishoni uliwasomba,
ule mto wa zamani, mto wa Kishoni.
Songa mbele, ee nafsi yangu,
kwa ujasiri!
22 Ndipo kwato za farasi zikafanya mshindo:
farasi wake wenye nguvu
huenda mbio kwa kurukaruka.
23 Malaika wa Bwana akasema, ‘Merozi alaaniwe.
Walaaniwe watu wake kwa uchungu,
kwa kuwa hawakuja kumsaidia Bwana,
kumsaidia Bwana dhidi ya hao wenye nguvu.’
24 “Yaeli abarikiwe kuliko wanawake wote,
mkewe Heberi, Mkeni,
abarikiwe kuliko wanawake wote
waishio kwenye mahema.
25 Aliomba maji, naye akampa maziwa;
kwenye bakuli la heshima
akamletea maziwa mgando.
26 Akanyoosha mkono wake
akashika kigingi cha hema,
mkono wake wa kuume
ukashika nyundo ya fundi.
Akampiga Sisera kwa nyundo,
akamponda kichwa chake,
akamvunjavunja na kumtoboa
paji lake la uso.
27 Aliinama miguuni pa Yaeli,
akaanguka; akalala hapo.
Pale alipoinama miguuni pake,
alianguka;
pale alipoinamia, ndipo alipoanguka,
akiwa amekufa.
28 “Kupitia dirishani mamaye Sisera alichungulia;
nyuma ya dirisha alilia, akasema,
‘Mbona gari lake linachelewa kufika?
Mbona vishindo vya magari yake
vimechelewa?’
29 Wanawake wenye busara
kuliko wengine wote wakamjibu;
naam, husema moyoni mwake,
30 ‘Je, hawapati na kugawanya nyara:
msichana mmoja au wawili kwa kila mtu,
mavazi ya rangi mbalimbali kwa Sisera kuwa nyara,
mavazi ya rangi mbalimbali yaliyotariziwa,
mavazi yaliyotariziwa vizuri kwa ajili ya shingo yangu:
yote haya yakiwa nyara?’
31 “Adui zako wote na waangamie, Ee Bwana!
Bali wote wakupendao na wawe kama jua
lichomozavyo kwa nguvu zake.”
Hivyo nchi ikawa na amani kwa miaka arobaini.