42
Mtumishi Wa Bwana
1 “Huyu hapa mtumishi wangu, ninayemtegemeza,
mteule wangu, ambaye ninapendezwa naye;
nitaweka Roho yangu juu yake,
naye ataleta haki kwa mataifa.
2 Hatapaza sauti wala kupiga kelele,
wala hataiinua sauti yake barabarani.
3 Mwanzi uliopondeka hatauvunja,
na utambi unaofuka moshi hatauzima.
Kwa uaminifu ataleta haki,
4 hatazimia roho wala kukata tamaa,
mpaka atakaposimamisha haki juu ya dunia.
Visiwa vitaweka tumaini lao katika sheria yake.”
5 Hili ndilo asemalo Mungu, Bwana,
yeye aliyeziumba mbingu na kuzitanda,
aliyeitandaza dunia na vyote vitokavyo humo,
awapaye watu wake pumzi,
na uzima kwa wale waendao humo:
6 “Mimi, Bwana, nimekuita katika haki;
nitakushika mkono wako.
Nitakulinda na kukufanya
kuwa Agano kwa ajili ya watu
na nuru kwa Mataifa,
7 kuwafungua macho wale wasioona,
kuwaacha huru kutoka kifungoni waliofungwa jela,
na kuwafungua kutoka gerezani
wale wanaokaa gizani.
8 “Mimi ndimi Bwana; hilo ndilo Jina langu!
Sitampa mwingine utukufu wangu
wala sanamu sifa zangu.
9 Tazama, mambo ya kwanza yametokea,
nami natangaza mambo mapya;
kabla hayajatokea
nawatangazia habari zake.”
Wimbo Wa Kumsifu Bwana
10 Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
sifa zake toka miisho ya dunia,
ninyi mshukao chini baharini,
na vyote vilivyomo ndani yake,
enyi visiwa na wote wakaao ndani yake.
11 Jangwa na miji yake na vipaze sauti zao;
makao anamoishi Kedari na yashangilie.
Watu wa Sela waimbe kwa furaha,
na wapige kelele kutoka vilele vya milima.
12 Wampe Bwana utukufu,
na kutangaza sifa zake katika visiwa.
13 Bwana ataenda kama mtu mwenye nguvu,
kama shujaa atachochea shauku yake,
kwa kelele ataamsha kilio cha vita,
naye atashinda adui zake.
14 “Kwa muda mrefu nimenyamaza kimya,
nimekaa kimya na kujizuia.
Lakini sasa, kama mwanamke wakati wa kujifungua,
ninapiga kelele, ninatweta na kushusha pumzi.
15 Nitaharibu milima na vilima
na kukausha mimea yako yote;
nitafanya mito kuwa visiwa
na kukausha mabwawa.
16 Nitawaongoza vipofu kwenye njia ambayo hawajaijua,
kwenye mapito wasiyoyazoea nitawaongoza;
nitafanya giza kuwa nuru mbele yao,
na kufanya mahali palipoparuza kuwa laini.
Haya ndiyo mambo nitakayofanya;
mimi sitawaacha.
17 Lakini wale wanaotumaini sanamu,
wanaoviambia vinyago, ‘Ninyi ndio miungu yetu,’
watarudishwa nyuma kwa aibu kubwa.
Israeli Kipofu Na Kiziwi
18 “Sikieni, enyi viziwi;
tazameni, enyi vipofu, mpate kuona!
19 Ni nani aliye kipofu isipokuwa mtumishi wangu,
na kiziwi kama mjumbe ninayemtuma?
Ni nani aliye kipofu kama yeye aliyejitoa kwangu,
aliye kipofu kama mtumishi wa Bwana?
20 Mmeona vitu vingi, lakini hamkuzingatia;
masikio yenu yako wazi, lakini hamsikii chochote.”
21 Ilimpendeza Bwana
kwa ajili ya haki yake
kufanya sheria yake kuwa kuu na tukufu.
22 Lakini hili ni taifa lililoibwa na kutekwa nyara,
wote wamenaswa katika mashimo,
au wamefichwa katika magereza.
Wamekuwa nyara,
wala hapana yeyote awaokoaye.
Wamefanywa mateka,
wala hapana yeyote asemaye, “Warudishe.”
23 Ni nani miongoni mwenu atakayesikiliza hili,
au atakayezingatia kwa makini katika wakati ujao?
24 Ni nani aliyemtoa Yakobo kuwa mateka,
na Israeli kwa wateka nyara?
Je, hakuwa yeye, Bwana,
ambaye tumetenda dhambi dhidi yake?
Kwa kuwa hawakufuata njia zake,
hawakutii sheria zake.
25 Hivyo akawamwagia hasira yake inayowaka,
ukali wa vita.
Iliwazunguka kwa miali ya moto, lakini hata hivyo hawakuelewa;
iliwateketeza, lakini hawakuyatia moyoni.