31
Mwerezi Katika Lebanoni
1 Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa tatu, siku ya kwanza, neno la Bwana likanijia, kusema: 2 “Mwanadamu, mwambie Farao mfalme wa Misri na makundi yake ya wajeuri:
“ ‘Je, ni nani awezaye kulinganishwa
na wewe katika fahari.
3 Angalia Ashuru, wakati fulani ilikuwa mwerezi huko Lebanoni,
ukiwa na matawi mazuri ukitia msitu kivuli;
ulikuwa mrefu sana,
kilele chake kilipita majani ya miti yote.
4 Maji mengi yaliustawisha,
chemchemi zenye maji mengi ziliufanya urefuke;
vijito vyake vilitiririka pale
ulipoota pande zote
na kupeleka mifereji yake
kwenye miti yote ya shambani.
5 Hivyo ukarefuka
kupita miti yote ya shambani;
vitawi vyake viliongezeka
na matawi yake yakawa marefu,
yakitanda kwa sababu ya wingi wa maji.
6 Ndege wote wa angani
wakaweka viota kwenye vitawi vyake,
wanyama wote wa shambani
wakazaana chini ya matawi yake,
mataifa makubwa yote
yaliishi chini ya kivuli chake.
7 Ulikuwa na fahari katika uzuri,
ukiwa na matawi yaliyotanda,
kwa kuwa mizizi yake ilikwenda chini
mpaka kwenye maji mengi.
8 Mierezi katika bustani ya Mungu
haikuweza kushindana nao,
wala misunobari haikuweza
kulingana na vitawi vyake,
wala miaramoni
haikulinganishwa na matawi yake,
wala hakukuwa na mti katika bustani ya Mungu
wa kulinganisha na uzuri wake.
9 Niliufanya kuwa mzuri
ukiwa na matawi mengi,
ulionewa wivu na miti yote ya Edeni
katika bustani ya Mungu.
10 “ ‘Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa sababu ulikuwa mrefu sana, kilele chake kikiwa juu ya majani manene ya miti na kwa sababu ulikuwa na kiburi cha urefu wake, 11 niliutia mikononi mwa mtawala wa mataifa, ili yeye aushughulikie sawasawa na uovu wake. Nikaukatilia mbali, 12 nayo mataifa mageni yaliyo makatili sana yaliukata huo mti na kuuacha. Matawi yake yalianguka juu ya milima na kwenye mabonde yote, vitawi vyake vikavunjika na kusambaa katika makorongo yote ya nchi. Mataifa yote ya duniani yakaondoka kutoka kwenye kivuli chake na kuuacha. 13 Ndege wote wa angani wakakaa kwenye ule mti ulioanguka na wanyama pori wote wakakaa katikati ya vitawi vyake. 14 Kamwe hakutakuwa na miti mingine kando ya hayo maji itakayorefuka zaidi ya huo, vilele vyake vikiwa juu ya majani yote ya miti. Hakuna miti mingine, hata kama imekunywa maji vizuri namna gani, itakayofikia urefu huo. Yote mwisho wake ni kifo, na kuingia ardhini, kama vile ilivyo kwa wanadamu, pamoja na wale waendao shimoni.
15 “ ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Katika siku ile mwerezi uliposhushwa chini kaburini* Yaani Kuzimu, Sheol kwa Kiebrania; pia mstari 16, 17. nilizifunika chemchemi zenye maji mengi kwa maombolezo: Nilivizuia vijito vyake na wingi wa maji yake nikauzuia. Kwa sababu yake niliivika Lebanoni huzuni, nayo miti yote ya shambani ikanyauka. 16 Niliyafanya mataifa yatetemeke kwa kishindo cha kuanguka kwake wakati nilipoushusha chini kaburini pamoja na wale washukao shimoni. Ndipo miti yote ya Edeni, miti iliyo bora kuliko yote na iliyo mizuri sana ya Lebanoni, miti yote ile iliyokunywa maji vizuri, ilifarijika hapa duniani. 17 Wale walioishi katika kivuli chake, wale walioungana naye miongoni mwa mataifa, nao pia walikuwa wamezikwa pamoja naye, wakiungana na wale waliouawa kwa upanga.
18 “ ‘Ni miti ipi ya Edeni inayoweza kulinganishwa nawe kwa fahari na utukufu? Hata hivyo, wewe pia, utashushwa chini pamoja na miti ya Edeni mpaka kuzimu, utalala miongoni mwa wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga.
“ ‘Huyu ni Farao pamoja na makundi yake yote ya wajeuri, asema Bwana Mwenyezi.’ ”