14
Shauri La Kumuua Yesu
(Mathayo 26:1-5; Luka 22:1-2; Yohana 11:45-53)
Zilikuwa zimebaki siku mbili tu kabla ya Sikukuu ya Pasaka, na Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwa wakitafuta njia ya kumkamata Yesu kwa hila na kumuua. Lakini walisema, “Tusilifanye jambo hili wakati wa Sikukuu, maana watu wanaweza wakafanya ghasia.”
Yesu Kupakwa Mafuta Huko Bethania
(Mathayo 26:6-13; Yohana 12:1-8)
Yesu alikuwa Bethania nyumbani kwa Simoni aliyekuwa na ukoma. Wakati alipokuwa ameketi mezani akila chakula cha jioni, mwanamke mmoja aliingia akiwa na chupa ya marhamu yenye manukato ya nardo* Nardo ni aina ya manukato yaliyotengenezwa kutokana na mimea yenye mizizi inayotoa harufu nzuri. safi ya thamani kubwa. Akaivunja hiyo chupa, akamiminia hayo manukato kichwani mwa Yesu.
Baadhi ya watu waliokuwepo pale walikuwa wakisemezana wao kwa wao, “Upotevu huu wote ni wa nini? Mafuta haya yangeweza kuuzwa kwa zaidi ya dinari Dinari 300 ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku 300. 300, na fedha hizo wakapewa maskini.” Wakamkemea vikali huyo mwanamke.
Lakini Yesu akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mwanamke? Mwacheni! Yeye amenitendea jambo zuri sana. Maskini mtakuwa nao siku zote na mnaweza kuwasaidia wakati wowote mnaotaka. Lakini mimi hamtakuwa nami siku zote. Huyu mwanamke amenitendea lile aliloweza. Ameumiminia mwili wangu manukato ili kuniandaa kwa maziko yangu. Amin, nawaambia, mahali popote ulimwenguni ambapo Injili itahubiriwa, jambo hili alilolitenda huyu mwanamke litatajwa pia kwa ukumbusho wake.”
Yuda Akubali Kumsaliti Yesu
(Mathayo 26:14-16; Luka 22:3-6)
10 Kisha Yuda Iskariote, mmoja wa wale wanafunzi kumi na wawili, akaenda kwa viongozi wa makuhani ili kumsaliti Yesu kwao. 11 Walifurahi sana kusikia jambo hili na wakaahidi kumpa fedha. Hivyo yeye akawa anatafuta wakati uliofaa wa kumsaliti.
Yesu Ala Pasaka Na Wanafunzi Wake
(Mathayo 26:17-25; Luka 22:7-14, 21-23; Yohana 13:21-30)
12 Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, siku ambayo kwa desturi mwana-kondoo wa Pasaka huchinjwa, wanafunzi wa Yesu wakamuuliza, “Unataka twende wapi ili tukuandalie mahali pa kula Pasaka?”
13 Basi akawatuma wawili miongoni mwa wanafunzi wake, akawaambia, “Nendeni mjini. Huko mtakutana na mwanaume amebeba mtungi wa maji. Mfuateni. 14  Mwambieni mwenye nyumba ile atakayoingia, ‘Mwalimu anauliza: Kiko wapi chumba changu cha wageni, ambamo mimi na wanafunzi wangu tutakula Pasaka?’ 15  Atawaonyesha chumba kikubwa ghorofani, kilichopambwa tena kilicho tayari. Tuandalieni humo.”
16 Wale wanafunzi wakaondoka na kwenda mjini, nao wakakuta kila kitu kama Yesu alivyowaambia. Hivyo wakaiandaa Pasaka.
17 Ilipofika jioni, Yesu akaja pamoja na wale wanafunzi wake kumi na wawili. 18 Walipoketi mezani wakila, Yesu akawaambia, “Amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti, mmoja anayekula pamoja nami.”
19 Wakaanza kuhuzunika na kumuuliza mmoja baada ya mwingine, “Je, ni mimi Bwana?”
20 Akawajibu, “Ni mmoja miongoni mwenu ninyi kumi na wawili, yule anayechovya mkate kwenye bakuli pamoja nami. 21  Mwana wa Adamu anaenda zake kama vile alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu yule amsalitiye Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu huyo kama hangezaliwa.”
Kuanzishwa Kwa Meza Ya Bwana
(Mathayo 26:26-30; Luka 22:14-20; 1 Wakorintho 11:23-25)
22 Walipokuwa wanakula, Yesu akachukua mkate, akashukuru, akaumega na kuwapa wanafunzi wake, akisema, “Twaeni mle; huu ndio mwili wangu.”
23 Kisha akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, nao wote wakanywa kutoka humo.
24 Akawaambia, “Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi. 25  Amin, nawaambia, sitakunywa tena katika uzao wa mzabibu, hadi siku ile nitakapounywa mpya katika Ufalme wa Mungu.”
26 Walipokwisha kuimba wimbo, wakatoka wakaenda Mlima wa Mizeituni.
Yesu Atabiri Kuwa Petro Atamkana
(Mathayo 26:31-35; Luka 22:31-34; Yohana 13:36-38)
27 Yesu akawaambia, “Ninyi nyote mtaniacha, kwa maana imeandikwa:
“ ‘Nitampiga mchungaji,
nao kondoo watatawanyika.’
28  Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.”
29 Petro akasema, “Hata kama wengine wote watakuacha, mimi sitakuacha.”
30 Yesu akamwambia, “Amin, nakuambia; leo, usiku huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, wewe mwenyewe utanikana mara tatu.”
31 Lakini Petro akasisitiza zaidi, “Hata kama itabidi kufa pamoja nawe, sitakukana kamwe.” Nao wale wengine wote wakasema vivyo hivyo.
Yesu Aomba Katika Bustani Ya Gethsemane
(Mathayo 26:36-46; Luka 22:39-46)
32 Wakaenda mahali paitwapo Gethsemane. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa, nami niende nikaombe.” 33 Kisha akawachukua pamoja naye Petro, Yakobo na Yohana. Akaanza kuhuzunika sana na kutaabika. 34 Akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe.”
35 Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba kwamba kama ingewezekana saa hiyo ya mateso imwondokee. 36 Akasema, “ Abba, Abba ni neno la Kiaramu ambalo maana yake ni Baba; ni mtoto wa kuzaa tu angeweza kulitumia kwa baba yake.Baba, mambo yote yawezekana kwako. Niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali vile upendavyo wewe.”
37 Akarudi kwa wanafunzi wake, akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, “Simoni, umelala? Je, hukuweza kukesha hata kwa saa moja? 38  Kesheni na mwombe, msije mkaingia majaribuni. Roho iko radhi, lakini mwili ni mdhaifu.”
39 Akaenda tena kuomba, akisema maneno yale yale. 40 Aliporudi, akawakuta tena wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito. Nao hawakujua la kumwambia.
41 Akaja mara ya tatu, akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Imetosha! Saa imewadia. Tazameni, Mwana wa Adamu anasalitiwa na kutiwa mikononi mwa wenye dhambi. 42  Inukeni, twende zetu! Tazameni, msaliti wangu yuaja!”
Yesu Akamatwa
(Mathayo 26:47-56; Luka 22:47-53; Yohana 18:3-12)
43 Yesu alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale wanafunzi Kumi na Wawili, akatokea. Alikuwa amefuatana na umati wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani, walimu wa sheria, na wazee.
44 Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni, mkamchukue chini ya ulinzi.” 45 Mara Yuda akamjia Yesu na kusema, “Rabi.”§ Rabi ni neno la Kiebrania ambalo maana yake ni daktari, mwalimu au bwana. Walikuwa na madaraja matatu: La chini kabisa Rab (bwana), la pili Rabi (bwana wangu), na la juu kabisa Raboni (mkuu wangu, bwana wangu mkuu). Akambusu. 46 Wale watu wakamkamata Yesu, wakamweka chini ya ulinzi. 47 Ndipo mmoja wa wale waliokuwa wamesimama karibu aliuchomoa upanga wake na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio.
48 Kisha Yesu akawaambia, “Mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyangʼanyi? 49  Siku kwa siku nilikuwa pamoja nanyi nikifundisha Hekaluni, wala hamkunikamata. Lakini Maandiko sharti yatimie.” 50 Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha, wakakimbia.
51 Kijana mmoja, ambaye hakuwa amevaa kitu isipokuwa alijitanda nguo ya kitani, alikuwa akimfuata Yesu. Walipomkamata, 52 alikimbia uchi, akaliacha vazi lake.
Yesu Mbele Ya Baraza La Wayahudi
(Mathayo 26:57-68; Luka 22:54-71; Yohana 18:13-24)
53 Wakampeleka Yesu kwa kuhani mkuu, nao viongozi wa makuhani wote, na wazee na walimu wa sheria wote wakakusanyika pamoja. 54 Petro akamfuata kwa mbali, hadi uani kwa kuhani mkuu. Huko akaketi pamoja na walinzi, akiota moto.
55 Viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi* Baraza la Wayahudi hapa ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa ndilo baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi, lililoundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu. lote wakatafuta ushahidi dhidi ya Yesu ili wapate kumuua. Lakini hawakupata jambo lolote. 56 Wengi walitoa ushahidi wa uongo dhidi yake, lakini maelezo yao hayakukubaliana.
57 Ndipo wengine wakasimama wakatoa ushahidi wa uongo dhidi yake, wakisema: 58 “Sisi tulimsikia akisema, ‘Mimi nitalibomoa Hekalu hili lililojengwa na wanadamu, na katika siku tatu nitajenga jingine ambalo halikujengwa na wanadamu.’ ” 59 Lakini hata hivyo, ushahidi wao haukukubaliana.
60 Basi kuhani mkuu akasimama mbele yao, akamuuliza Yesu, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?” 61 Lakini Yesu akakaa kimya, hakusema neno lolote.
Kuhani mkuu akamuuliza tena, “Je, wewe ndiwe Kristo, Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. Mwana wa Mungu Aliyebarikiwa?”
62 Yesu akajibu, “Mimi ndimi. Nanyi mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.”
63 Kuhani mkuu akararua mavazi yake, akasema, “Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi? 64 Ninyi mmesikia hayo makufuru. Uamuzi wenu ni gani?”
Wote wakamhukumu kwamba anastahili kifo. 65 Kisha baadhi ya watu wakaanza kumtemea mate; wakamfunga kitambaa machoni, wakampiga kwa ngumi na kumwambia, “Tabiri!” Walinzi wakamchukua na kumpiga makofi.
Petro Amkana Yesu
(Mathayo 26:69-75; Luka 22:56-62; Yohana 18:15-18, 25-27)
66 Petro alipokuwa bado yuko chini kwenye ua wa jumba la kifalme, tazama akaja mmoja wa watumishi wa kike wa kuhani mkuu. 67 Alipomwona Petro akiota moto, akamtazama sana, akamwambia,
“Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu, Mnazareti.”
68 Lakini Petro akakana, akasema, “Sijui wala sielewi unalosema.” Naye akaondoka kuelekea kwenye njia ya kuingilia.
69 Yule mtumishi wa kike alipomwona mahali pale, akawaambia tena wale waliokuwa wamesimama hapo, “Huyu mtu ni mmoja wao.” 70 Lakini Petro akakana tena.
Baada ya muda kidogo wale waliokuwa wamesimama hapo karibu na Petro wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana wewe pia ni Mgalilaya!” 71 Petro akaanza kujilaani na kuwaapia, “Mimi simjui huyu mtu mnayesema habari zake!”
72 Papo hapo jogoo akawika mara ya pili. Ndipo Petro akakumbuka lile neno Yesu alikuwa amemwambia: “Kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.” Akavunjika moyo, akalia sana.

*14:3 Nardo ni aina ya manukato yaliyotengenezwa kutokana na mimea yenye mizizi inayotoa harufu nzuri.

14:5 Dinari 300 ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku 300.

14:36 Abba ni neno la Kiaramu ambalo maana yake ni Baba; ni mtoto wa kuzaa tu angeweza kulitumia kwa baba yake.

§14:45 Rabi ni neno la Kiebrania ambalo maana yake ni daktari, mwalimu au bwana. Walikuwa na madaraja matatu: La chini kabisa Rab (bwana), la pili Rabi (bwana wangu), na la juu kabisa Raboni (mkuu wangu, bwana wangu mkuu).

*14:55 Baraza la Wayahudi hapa ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa ndilo baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi, lililoundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu.

14:61 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.