11
Pigo La Kumi: Kuuawa Wazaliwa Wa Kwanza
Basi Bwana alikuwa amemwambia Mose, “Nitaleta pigo moja zaidi kwa Farao na katika nchi ya Misri. Baada ya hilo, atawaacha mwondoke hapa na atakapofanya hivyo, atawafukuza mtoke kabisa. Waambie watu wote waume kwa wake wawaombe majirani zao vitu vya fedha na vya dhahabu.” (Bwana akawafanya Wamisri wawe na moyo wa ukarimu kwa Waisraeli, naye Mose mwenyewe akaheshimiwa sana na maafisa wa Farao na watu wote katika nchi ya Misri.)
Kwa hiyo Mose akasema, “Hili ndilo Bwana asemalo: ‘Panapo usiku wa manane Mimi nitapita katika nchi yote ya Misri. Kila mwanaume kifungua mimba katika Misri atakufa, kuanzia mzaliwa wa kwanza wa kiume wa Farao, aketiye penye kiti cha ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa kiume wa mtumwa wa kike, anayesaga nafaka kwa jiwe, pamoja na kila mzaliwa wa kwanza wa mifugo. Patakuwepo kilio kikubwa katika nchi yote ya Misri, kilio kibaya ambacho hakijakuwepo wala kamwe hakitakuwepo tena. Lakini miongoni mwa Waisraeli hakuna hata mbwa atakayembwekea mwanadamu wala mnyama yeyote.’ Ndipo mtakapojua kuwa Bwana huweka tofauti kati ya Misri na Israeli. Maafisa hawa wako wote watanijia, wakisujudu mbele yangu, wakisema, ‘Ondoka, wewe pamoja na watu wako wote wanaokufuata!’ Baada ya haya nitaondoka.” Kisha Mose, huku akiwa amewaka hasira, akamwacha Farao.
Bwana alikuwa amemwambia Mose, “Farao atakataa kukusikiliza, ili maajabu yangu yapate kuongezeka katika nchi ya Misri.” 10 Mose na Aroni wakafanya maajabu haya yote mbele ya Farao, lakini Bwana akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, wala hakuwaachia Waisraeli waondoke katika nchi yake.