26
Uzia Mfalme Wa Yuda
(2 Wafalme 14:21-22; 15:1-7)
1 Kisha watu wote wa Yuda wakamtwaa Uzia, aliyekuwa na umri wa miaka kumi na sita, nao wakamfanya mfalme mahali pa Amazia baba yake. 2 Ndiye alijenga upya Elathi kuirudisha kwa Yuda baada ya Amazia kulala pamoja na baba zake.
3 Uzia alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka hamsini na miwili. Mama yake aliitwa Yekolia wa Yerusalemu. 4 Akatenda yaliyo mema machoni pa Bwana, kama Amazia baba yake alivyofanya. 5 Akamtafuta Mungu katika siku za Zekaria, aliyemwelekeza kumcha Mungu. Wakati wote alipomtafuta Bwana, Mungu alimfanikisha.
6 Alipigana vita dhidi ya Wafilisti na kubomoa kuta za Gathi, Yabne na Ashdodi. Kisha akajenga upya miji karibu na Ashdodi na mahali pengine katikati ya Wafilisti. 7 Mungu akamsaidia dhidi ya Wafilisti na dhidi ya Waarabu walioishi Gur-Baali na dhidi ya Wameuni. 8 Waamoni wakamletea Uzia ushuru, umaarufu wake ukaenea hadi kwenye mpaka wa Misri, kwa sababu alikuwa amekuwa na nguvu sana.
9 Uzia akajenga minara huko Yerusalemu katika Lango la Pembeni, katika Lango la Bondeni na katika pembe, mahali kuta zikutanapo, kisha akaijengea ngome. 10 Akajenga pia minara jangwani na kuchimba visima vingi vya maji, kwa sababu alikuwa na mifugo mingi chini ya vilimani na kwenye nchi tambarare. Alikuwa na watu wanaofanya kazi katika mashamba yake na kwenye mashamba yake ya mizabibu huko vilimani na katika ardhi zenye rutuba, kwa kuwa aliupenda udongo.
11 Zaidi ya hayo, Uzia alikuwa na jeshi lililofunzwa vizuri, lililokuwa tayari kwenda vitani kwa vikosi kufuatana na idadi yao kama walivyokusanywa na Yeieli mwandishi na Maaseya msimamizi chini ya maelekezo ya Hanania, mmojawapo wa maafisa wa mfalme. 12 Idadi yote ya viongozi wa jamaa waliowaongoza hawa wapiganaji walikuwa 2,600. 13 Chini ya uongozi wao kulikuwa na jeshi la askari 307,500 watu waliofundishwa kwa ajili ya vita, jeshi lenye nguvu la kumsaidia mfalme dhidi ya adui zake. 14 Uzia akalipatia jeshi lote ngao, mikuki, chapeo, dirii, pinde na mawe ya kombeo. 15 Huko Yerusalemu watu wenye utaalamu mkubwa wakatengeneza mitambo iliyotumika katika minara na kwenye pembe za ulinzi ili kurusha mishale na kuvurumisha mawe makubwa. Sifa zake zikaenea mbali sana kwa sababu alisaidiwa mno mpaka akawa na nguvu sana.
16 Lakini baada ya Uzia kuwa na nguvu sana, majivuno yake yakamsababishia kuanguka. Alikosa uaminifu kwa Bwana Mungu wake, naye akaingia hekaluni mwa Bwana ili afukize uvumba kwenye madhabahu ya kufukizia uvumba. 17 Azaria kuhani akiwa pamoja na makuhani wengine themanini wa Bwana wenye ujasiri wakamfuata huko ndani. 18 Wakamkabili na kumwambia, “Siyo sawa kwako, Uzia, kumfukizia Bwana uvumba. Hiyo ni kazi ya makuhani, wazao wa Aroni, ambao wamewekwa wakfu ili kufukiza uvumba. Ondoka mahali patakatifu, kwa kuwa umekosa uaminifu nawe hutaheshimiwa na Bwana.”
19 Uzia, ambaye alikuwa na chetezo mkononi mwake tayari kufukiza uvumba, akakasirika. Alipokuwa anawaghadhibikia makuhani mbele ya madhabahu ya kufukizia uvumba katika Hekalu la Bwana, ukoma ukamtokea penye kipaji chake cha uso. 20 Azaria kuhani mkuu pamoja na makuhani wengine wote walipomtazama wakaona kwamba alikuwa na ukoma penye kipaji chake cha uso wakaharakisha kumtoa nje. Naam, hata yeye mwenyewe alikuwa anatamani kuondoka kwa sababu Bwana alikuwa amempiga.
21 Mfalme Uzia alikuwa na ukoma mpaka siku ya kufa kwake. Akatengwa katika nyumba ya pekee akiwa mwenye ukoma, naye akawa ametengwa kutoka Hekalu la Bwana. Yothamu mwanawe akawa msimamizi wa jumba la mfalme, pia akawaongoza watu wa nchi.
22 Matukio mengine ya utawala wa Uzia, kuanzia mwanzo mpaka mwisho, yameandikwa na nabii Isaya mwana wa Amozi. 23 Uzia akalala pamoja na baba zake, naye akazikwa karibu nao katika shamba la kuzikia lililokuwa mali ya wafalme, kwa kuwa watu walisema, “Alikuwa na ukoma.” Yothamu mwanawe akawa mfalme baada yake.